Mwandishi Wetu
MSHTUKO! Staa wa muziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’
amefunguka siri nzito kwa mashabiki waliokuwa wakimpigia kampeni katika
mitandao mbalimbali ili ashindwe kwenye Tuzo za MTV Africa Music (Mama)
2015, zilizofanyika usiku wa kuamkia Jumapili iliyopita huko Durban,
Afrika Kusini baada ya kushinda tuzo moja na kudai kuwa ni aibu kwa
waliokuwa wakifanya kampeni asishinde.
Diamond akiwa katika red carpet ya tuzo hizo.
DIAMOND MTUMBUIZAJI BORA AFRIKA
Diamond alitwaa Tuzo ya Best Live Act (Mtumbuizaji Bora Afrika) ambapo
alijikuta akifurahi kupindukia huku akiwakejeli wale waliokuwa
wakimpigia kampeni ashindwe kwamba bado ataendelea kuwakalisha vibaya.
WAMEBAKI NA AIBU
“Nina furaha sana kupata tuzo tena, wale waliokuwa wakipiga kampeni
kwenye mitandao kwamba nisipigiwe kura naona wamebaki na aibu yaani
nimewaumbua, hapa bado ninaongeza nguvu zaidi na nina mpango wa kufanya
kazi na mastaa wakubwa wa Marekani, ila ninawashukuru wale walionipigia
kura,” alisema Diamond.
JOKATE ALALAMIKA KUDHALILISHWA
Wakati Diamond akisherehekea ushindi huo, mwanadada aliyewahi kuwa
mpenzi wake, Jokate Mwegelo ‘Kidoti’ amelalamika kudhalilishwa mtandaoni
na mwanamuziki huyo baada ya kuweka video akiwa anacheza wimbo wa jamaa
huyo wa Mdogo Mdogo na kuambatanisha na maneno yaliyosomeka: “Mbona
bado. Mtanyooka tu.”
Jokate.
“Sijapenda na sijawahi kuona mwanaume mswahili kama Diamond,
anatafuta kiki za ajabu tu mjini hapa kwani hiyo video ni ya zamani tena
nilipigwa nikiwa studio lakini nimeshangazwa sana na kitendo chake cha
kuweka kwenye ukurasa wake wa Instagram na kuambatanisha na maneno ya
kunidhalilisha,” alisema Jokate akiwa amepaniki.
Diamond alipata mapokezi ya kifalme baada ya kutua kwenye Uwanja wa
Kimataifa Ndege wa Julius Nyerere, Dar, Jumapili iliyopita ambapo kundi
kubwa la watu lilijitokeza kumpokea pamoja na mama yake mzazi, Sanura
Kassim ‘Sandra’ ambaye kwa muda mrefu alikuwa mgonjwa lakini alionekana
akimfurahia mwanaye uwanjani hapo.
Baada ya kutua Bongo, Diamond alifikishiwa malalamiko ya Jokate
kwamba alikuwa amemdhalilisha yeye na wanawake wengine ambapo
aliyafungukia:
“Unajua, kwanza nimecheka alafu nimesikitishwa kwa sababu nimeambiwa
sijasoma, nimeambiwa kuna posti ameandika (Jokate), amezungumzia vitu
vingi…Yeye kacheza kama fan wa nyimbo zangu na mimi nilimposti kama fan
wangu.
“Hakuna mahali nilimuandika jina, kwa nini achukulie vibaya?
“Ukiona mtu anajishuku ujue kuna namna nyuma. Mbona mimi naposti watu
wengi tu, tena naandika caption zangu za vitukovituko maana yake mimi
nina caption za vituko.
“Ni kweli mimi ni mswahili, nimezaliwa Tandale, nimekulia Tandale na Tandale ndiyo kumenifanya leo niwe hapa nilipo…
“Kwa hiyo nina caption zangu za uswahili kwa sababu uswahili ndiyo
umenikuza…siziachi kuziandika, huwa naziandika nyingi ..kwa nini ya
kwake yeye tu aione tatizo?
Ali kiba.
“Kwani kuna ubaya gani mimi kuandika mtanyooka tu kama yeye haimhusu ina maana labda kuna kitu kinamhusu.
“Nimeambiwa pia amezungumza kwamba ndiyo maana wanaogopa kuwasapoti
wasanii Watanzania kwa sababu wakiwasapoti wanadhalilishwa, yeye mimi
mpaka nimeenda kuchukua tuzo alinisapoti nini?
“Aliposti hata posti moja kusema mpigieni kura Diamond? Sasa hivi
anajishaua eti kanisapoti. Amesapoti nini? Eti ametoa hongera, mimi
nimeshinda tuzo, eti ooh hongera kwa tuzo by the way, angeposti
kuhamasisha watu wapige kura ili ushindi uje nyumbani.
“Lakini kwa chuki alizojazwa zisizo na sababu na roho mbaya
aliyowekewa na watu, imemfanya ashindwe hata kuniposti na kutengeneza
chuki za chinichini kwa kudhani wakiwapigia kura Wanigeria mimi nitakosa
tuzo…mimi nimeshinda, alafu anajifanya kutoa hongera, eti wanasapoti
muziki wa Kitanzania, ananisapoti nini, lini amenisapoti au ameona tuzo
imekuja ndiyo anajifanya kutoa hongera? Tuacheni unafiki.”
TUJIKUMBUSHE
Awali tuzo hizo zilivyotangazwa watu mbalimbali wakiwemo Timu Ali kiba
na wale mahasimu wake walikuwa wakipiga kura za kumpinga Diamond na
kumpigia kampeni msanii wa Nigeria, Davido, jambo ambalo mwanamuziki
huyo aliwataka kuachana nalo na kuangalia utaifa kwanza.
Miongoni mwa watu ambao hawakuwa wakimsapoti Diamond ni wapenzi wake
wa zamani, Wema Sepetu na Jokate ambapo Timu Wema na Timu Diamond
zilikuwa zikipambana kila kukicha kutokana na kila upande kumtaka
mshindi wao yaani Diamond na wengine wakimpigia kura Davido.